Kwa wapenzi wa RIWAYA hii inakuhusu kutoka "KALAMU YANGU",

on Friday, April 8, 2016 - No comments:

Ni Riwaya ya kusisimua sana yenye visa na matukio ya kweli. Nenda nayo sawa:
Kwa hadithi, riwaya, mashairi
tembelea www.kalamuyangu.blogspot.com

NITARUDI ARUSHA ....I
Hali ya hewa ya jiji la Arusha jioni hii ilikuwa ya ubaridi kama kawaida yake huku upepo ukisogeza wingu dogo la mvua kuelekea upande wa kasikazini magharibi na kuzuia adha ya mvua na kuleta karaha kwa wananchi na wafanyabiashara ambao mvua ilikuwa kero kwao licha ya kuwa wengi walikuwa wakifunga biashara zao.Taratibu nilijisogeza kwenye kituo kikubwa cha mabasi baada ya kuagana na rafiki yangu mpya ambaye nilikuja kuonana naye baada ya kufahamiana naye kwenye mtandao mmoja maarufu wa kijamii.
Hii ilikuwa safari yangu ya kwanza si kufika jijini Arusha , bali kusafiri kwa zaidi ya saa moja kwenda kuonana na rafiki wa kike ambaye ilikuwa imepita miezi nane tangu tuanze kuwasiliana kwenye mitandao wa kijamii kabla ya kupeana namba za simu na kupigiana simu.Japokuwa mwanzoni nilimtaka rafiki huyu aje Moshi ambako ndiko nilikokuwa nikisoma,lakini kwa msimamao wake wa kutomuamini mtu moja kwa moja nilijikuta nikikosa sababu za kutomfuata huko Arusha hasa baada ya kudai kuwa nilikuwa nimeshaanza kumpenda na kumwomba awe mpenzi wangu.
Kwangu ilikuwa ni mara ya kwanza pia kupata mpenzi ambaye alikuwa akitoka kwenye familia ya kitajiri sana , kwani kabla ya hapa wengi nilikuwa nikilingana nao uwezo wakati mwingine hata kuwazidi lakini kwa huyu niliyekuwa nimemfuata Arusha alikuwa amenizidi kila kitu kuanzia umri, kiwango cha elimu na hata kipato chake na cha wazazi wake.
Kwa uzuri wa asili naye hakuwa nyuma alijaaliwa rangi nyeusi isiyokolezwa ama kupunguzwa na kemikali yoyote huku nywele zake alizokuwa amezikata kwa mtindo wa kuziacha kidogo juu na kuzipunguza sana pembeni zikimfanya aonekane ni miongoni mwa vijana wa kisasa.Macho yake ya wastani yalikuwa kama yakinikonyeza kila aliponiangalia huku miguu yake ikionekana sehemu ndogo sana kwani ilikuwa imefunikwa na pensi jeupe chini akiwa na viatu vyepesi vya rangi nyeupe pia.
Midomo yake mikubwa haikurembwa na chochote zaidi ya kulainishwa na mate ambayo kila baada ya dakika kama kumi hivi yalifikishwa hapo na ulimi ambao ni kama alikuwa na kilema cha kuutafuna muda wote, kiasi kwamba nilifikiria kuwa kama angekuwa akiuremba mdomo wake basi urembo wote ungeishia kinywani kwa kupelekwa na ulimi wake ambao haukupenda kutulia.
Kwa kifupi kila sekunde iliyokuwa ikienda wakati nimekaa na huyo rafiki mpya basi nilikuwa nikigundua kitu kimoja kizuri alichokuwa amejaaliwa na mwenye kuumba vilivyo na visivyo na uhai.Alikuwa na uzuri ambao hata kuueleza nahisi sitoweza kwani nitakuwa ninasahau baadhi ya vitu vya kipekee vya dada huyo ambaye tofauti na ilivyozoeleka alinipeleka nyumbani kwake ambao alikaa na mdogo wake kabla ya kwenda nyumbani kwa wazazi wake ambako nako nilipokelewa kama rafiki mwema wa familia.
Mwanzoni nilipata shaka kufika kwa wazazi wake lakini alinitoa hofu kwa kunieleza kuwa alikuwa amewapa taarifa juu ya ujio wangu na hawakuwa na mawazo hasi juu ya urafiki wetu kwani wao ni miongoni mwa familia ambazo utandawazi kwao hauna athari nyingi hasi kiasi kwamba washindwe kujua nini maana ya urafiki.
Alidai pia sikuwa rafiki wa kwanza kwenda kwao kwani kuanzia alipokuwa shule ya msingi hadi alipopata shahada ya uhasibu alikuwa akipata na kupoteza marafiki wengi hivyo alijivunia sana kupata rafiki mpya.Safari na mizunguko yote hiyo tuliifanya kwa gari ambalo si kwa kunieleza bali kwa kuchunguza tuu nilihisi kuwa lilikuwa lake.
Jioni hiyo ilinikuta nikiwa miongoni mwa wasafiri wengi walikuwa wakiwahi magari ya kuwafikisha waendako huku wafanyabiashara licha ya wingu lile dogo kuhamishwa na upepo bado walikuwa na hofu ya mvua kunyesha hivyo walifungafunga na kuweka bidhaa zao vizuri hasa zile ambazo waliziweka nje ya vibanda na ofisi zao za biashara.Baada ya kuhakikisha kuwa nimepanda gari rafiki yangu huyo niliyemjua kwa majina ya Alice Josephat Temu alirudi garini na kunipungia mkono kisha aliondoka eneo lile akiogopa kusababisha foleni kwani haikuwa ni sehemu rasmi ya kuegesha magari madogo.
Baada ya dakika kama thelathini hivi taratibu gari nililopanda lilitoka nje ya kituo baada ya kuunguruma na kusogezwa kisha kurejeshwa kwa muda mrefu sana huku wapiga debe wakiumiza viganja vyao kwa kulibamiza makofi kwa muda mrefu sana.Baada ya kutoka kituoni gari lilingia kwenye njia kuu ya kutoka jijini lakini tulikuta foleni kubwa sana iliyokuwa imenitia hofu ya kuchelewa magari ya kunitoa Moshi mjini kunifikisha nilikokuwa nikiishi ambako ni nje ya mji huo uliokuwa ukisifika kwa usafi kwa kipindi fulani kilichopita.
Foleni iliifanya gari kusimama huku ikiunguruma, hapo ndipo nilipogundua kuwa aliyetutoa kituoni na kutufikisha pale hakuwa dereva bali kondakta wa lile gari kwani wakati tupo kwenye foleni nilishuhudia dereva akiingia garini na yule aliyekuwa akiiendesha gari alirudi upande ambao tulikaa abiria.
Naye baada ya kushilia usukani alijaribu kupita pembeni mwa barabara kukwepa ile foleni huku akipitisha gari sehemu ambazo zilikuwa zikitumiwa na waenda kwa miguu ,mara mbili nilishudhudia akisimamisha gari kwa ghafla akiwakosa kosa waendesha baiskeli ambao kwa jioni ile waliamua kutumia njia za waenda kwa miguu.Baadaye aliamua kusimamisha gari baada ya kuona askari wa usalama wa barabarani wakija upande wake , ambapo licha ya kusimama walimpa onyo kali.
Tukiwa kwenye foleni hiyo alipita kijana mmoja aliyekuwa akiomba fedha ya chakula kutoka kwa abiria waliokuwa kwenye magari, alikuwa akitembea kwa kuchechemea huku mwili wake ukionekana kuegemea upande mmoja kana kwamba alikuwa akiumia upande mmoja wa mwili wake hivyo kupunguza maumivu alikuwa akiupunguzia mzigo upande uliokuwa ukimuuma.Hakuwa mchafu kama wengi wa kundi lake walivyokuwa alionekana nadhifu sana baada ya kupigwa na mwanga wa magari yaliyokuwa kwenye foleni , shati lake la bluu bahari na suruali yake nyeusi ya kitambaa ambayo kwa haraka haraka licha ya kuwa ilikuwa safi yeyote angejua kuwa ilikuwa haijaonja pasi tangu ilipotolewa dukani.
Licha ya kuwa kulikuwa na ubaridi ambao hata kwa mtu aliyekuwa garini alikuwa akiuhisi ukigusa mifupa lakini yule kijana alikwa akitembea kana kwamba hakuihisi ile baridi huku shati lake likipepea na kuubana mwili wake ambao haukuwa na nguo nyingine chini ya lile shati.Nilikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa wakimfuatilia kwa macho yule kijana kwani hata alipolifikia gari letu wengi tuligeukia upande aliokuwa akianzia kuomba.
Nilimshuhudia kijana mmoja ambaye alikuwa amekaa mbele yangu akiwa amejifunika shuka la kimasai na msichana ambaye kwa harakaharaka nilihisi kuwa walikuwa wapenzi akimpa noti ya mia tano kutoka kwenye burungutu la pesa ambalo aliisaka sana hiyo mia tano, huku yule mwombaji akishukuru sana baada ya kupewa ile hela kabla ya kuhamia dirisha nililokuwa nimekaa ambapo kama kawaida aliomba hela ya chakula.
Hapo nilimwona kwa ukaribu na uzuri zaidi ,kumbe kabla sikuona kovu lililokuwa mdomoni mwake na kumfanya ongee kwa shinda kwani liliufanya mdomo wake ukae vibaya kidogo lakini aliponyanyua mdomo wake nilijua kuwa hakuwa na meno ya mbele, sikutaka kumwangalia zaidi kwani si tuu alinifanya nimwonee sana huruma bali alinifanya nimwogope kwani nilihisi natazamana na kiumbe fulani cha kutisha ambacho kilifanana sana na binadamu, kwa haraka haraka nikatoa noti ya shilingi elfu moja na kumpa.
Wakati nampatia hiyo noti nilikuja kugundua pia hakuwa na vidole vyote kwani mkono wake wa kushoto ulikuwa una kidole kimoja na mkono wake wa kulia ulikuwa umebaki kiganja tuu bila vidole.Nilijikuta nikisimka mwili wangu nikikwepesha macho kwake lakini nilijikuta nikimgeukia hata alipohamia kwenye dirisha la nyuma na nilipokaa.
Alizunguka karibu madirisha yote ya upande wetu na kuhamia upande mwingine akianzia nyuma ya lile gari ambapo alikutana na mzee mmoja ambaye kwa mwonekano wake nilimchukulia kama siyo mkurugenzi wa kampuni fulani basi alikuwa ni mwanasiasa ambaye alikuwa ameamua kutumia usafiri wa umma ajue kero zake akiiacha gari yake ama ya kampuni ipumzike.
‘’Nikusaidie ukale we mwanangu?’’Alipaza sauti na kuwafanya abiria wengine waungane na wachache tuliokuwa tukimfuatilia kwa macho yule kijana wa ajabu.
‘’Hapana baba naomba tuu nikapate chakula sijala tangu jana ndugu yangu’’Aliongea kwa taabu yule kijana.
‘’Hahaaaa , hivi wewe ni mtanzania kweli, maana nimekuuliza kwa Kiswahili sanifu kuwa wewe ni mwanangu bado unaniita baba yako, kama mama yako kakudanganya kuwa baba yako yupo kwenye hili gari basi kanifananisha tuu, nina watoto watatu tuu ambao nimewazaa ndani ya ndoa takatifu ambayo Nilifungishwa na Padre Karugendo mwaka themanini na saba sasa we mwanangu wa wapi? Haaaahahahaa watanzania bwana kwa mbinu za maisha ’’Alimalizia kwa kicheko yule mzee ambaye niliamua kumpa jina la Mwanasiasa.
Nilimwona yule kijana akilengwa na machozi baada ya pikipiki moja iliyokuwa ikitokea mbele yake kumumulika usoni, taratibu aliondoka na kusogea pembeni kuipisha ile pikipiki iliyommulika ipite.
‘’We mpumbavu nenda kaanzishe shamba la mchicha kijijini huko uje utuuzie tujenge afya si kuja kutunukia meno yako hapa, haya shika mtaji huo’’Aliongea yule Mwanasiasa akimtupia noti kadhaa za shilingi elfu kumi lakini kitu cha ajabu yule kijana ni kama alikuwa ameganda hakuongea wala kujongea hadi vijana kadhaa wa mjini wakiwemo makondakta wa magari yaliyokuwa kwenye foleni walianza kuzigombania zile noti.
Nilishuhudia Yule kijana akitoka eneo lile taratibu akionekana kuguswa na kitu fulani kilichokua kimemuumiza hadi alipopotea kwenye upeo wa mboni zangu.Nilijikuta nikimhurumia sana yule kijana ambaye niliamini kuwa alikuwa akiumia sana kwa maneno yale si tuu kutoka kwa yule Mwanasiasa bali yalitoka kwenye vinywa vya watu wengi wenye roho na akili kama ya Mwanasiasa kila siku alipokuwa kwenye harakati zake za kutafuta mlo.
Niliona kabisa hali yake kwa nje kuwa haikumruhusu kufanya kazi yoyote ngumu kutokana na umbo lake, nilihisi kuwa alikuwa akiteseka sana kutokana na hali yake ,hasa alipoambiwa kuwa alikuwa akinuka meno, ni kweli nilisikia harufu mbaya alipokuwa amesimama dirishani pangu lakini haikuwa ni harufu iliyotoka kinywani bali ni harufu ya kuoza sehemu ya mwili.
Nilijaribu kubashiri sababu ya kukutana na adha ile lakini kila nilipobashiri niliona kama angekutana na madhira niliyombashiria basi angekuwa mfu ama asingekuwa kwenye hali mbaya kama ile.Nilijikuta nikizama mawazoni peke yangu licha ya maongezi ya hapa na pale kumhusu yule kijana kuendelea garini.Kuna waliokuwa wakiungana na msimamo wa yule Mwanasiasa ambao walikuwa wengi na wachache sana walimpinga tena kwa kuaamua kukaa kimya huku wakijitambulisha kwa miguno na nyuso zao za huzuni.Wengi waliamua kutotoa msimamo wao kinyume na yule Mwanasiasa kwani kila aliyejaribu kunyanyua kinywa kupingana naye alikataliwa na wa upande wake ama yeye mwenyewe huku wakitoa mifano kadhaa.
Alianza yule kaka aliyekuwa amekaa mbele yangu huku akiwa amejifunika shuka la kimasai na ambaye nilihisi kuwa alikuwa ni mpenzi wake;
‘’Mie hao nawafahamu, kuna mama alikuwa akija pale UDSM yaani ye kila lecture alikuwa akiingia class na kuanza kupitisha daftari kuomba msaada akidai kuwa alikuwa mjane na alikuwa akisome…’’Hakumaliza yule kijana ambaye niliamua kupachika jina la Msomi wa Mlimani alikatishwa na sauti nyingine kutoka siti za nyuma.
‘’He! bado yupo hadi leo yule mama mie nakumbuka mwaka 2009 nilimwacha akiendelea kukusanya pesa nasikia anamiliki hoteli nyingi sana yule mama licha ya kuwa mjane kweli lakini anasaidiwa sana na watoto wake ambao wengi wana uwezo na wapo nje ya nchi’’ Aliongeza huyu mwingine ambaye niliamua kumpa jina la Mwana UDSM.
‘’Mmeona hawa ni wezi tuu , katumia ulemavu wake kaongezea na uchafu anakusanya hela zenu bila jasho, mtaishia kuwaita wanasiasa wezi wakati hela zenu mnaibiana wenyewe tena bila kodi’’Aliongea yule Mwanasiasa kwa madaha wakati huo gari ilikuwa imeshatoka kwenye foleni.
‘’We kweli mwanasiasa na unatetea wezi wenzako kwa kuwatumia hawa watu unataka kutuaminisha hawa ni wezi wakubwa kuliko walioiba kwenye RICHMOND au ESCROW? acheni hizo bwana’’Ilisikika sauti ya dada mmoja aliyekuwa jirani tuu na yule Mwanasiasa ambaye niliamua kumpa jina la UKAWA.
‘’Mnadanganywa na hao CHADEMA wenu muwaone wanasiasa ni wezi bila kujua kuwa hata hao chadema ni wanasiasa maadui wenu ni wengi sana wakiwa pamoja na hao wezi eti mtu anajaza daftari zima na kukusana pesa za wanachuo kila siku huku akimiliki hoteli mwisho wasiku wanachuo hao hao wanaandamana kudai kuongezewa hela na hao Chadema wanawaunga mkono bila kujua matumizi yenu mabaya, lakini mie wala siyo mwanasiasa na hata siipendi hiyo siasa mie ni mtaalamu bwana nawatibu watu’’Aliongea yule Mwanasiasa kwa madaha huku akiukana uanasiasa kwa kujitambulisha kuwa alikuwa tabibu.
‘’Kwani wewe kuwa tabibu ndo kunakuzuia kuwa mwanasiasa nakujua sana wewe nakuona pale KCMC nasikia ulikuwa umeshiriki sana kwenye mgomo wa madaktari waliokuwa wakidai pesa zao na kusababisha vifo vya mamia ya Watanzania nyie ni zaidi na hawa omba omba ambao hawamuumizi yeyote’’Aliongea dereva la gari akigeuka geuka kisha kurudisha umakini kwenye usukani.
‘’We dereva endesha gari na wewe unataka utuue hapa kisa siasa , ndio maana siwapendi wanasiasa ‘’Aliongea kwa unyonge yule Mwanasiasa wangu ambaye maneno ya dereva yalionekana kumchoma.
‘’Nyie mnasema omba omba hawamjeruhi mtu, mnadhani wanakula wapi wasipopewa wanachoomba?’’ Aliuliza yule niliyempachika jina la Mwana UDSM na kusababisha ukimya kwani hakuna aliyekuwa amenyanyua kinywa kwa dakika nzima, kisha akaendelea.
‘’Hao wakikosa pesa ya kula kwa kuomba huhamia kwenye kazi nyingine isiyo rasmi itegemeayo nguvu na kuanza kuwapora watu…’’Alifafanua Mwana UDSM, lakini alikatishwa na sauti ya binti mmoja aliyekuwa akibishana na kondakta kwenye siti za nyuma.
‘’Mie nimeuliza kwa kondakta nimeambiwa elfu mbili mia tano hadi Moshi sa hiyo elfu tatu inatoka wapi?’’ Aliongea yule binti akipaza sauti.
‘’Kondakta gani aliyekuambia hiyo bei usiku huu ?’’ Aliuliza yule kondakta kwa sauti iliyojaa kebehi na ya kumuaibisha yule binti ambaye wakati huo alikuwa amesimama , amefura kwa hasira.
‘’Si yule aliyetuleta kwenye gari , yenu isitoshe mchana nimekuja Arusha kwa elfu mbili mia tano kwa hiyo hiyo mia tano imeongezwa leo mchana?’’ Alihoji yule dada na kuwafanya watu waendelee kumtazama kwa mshangao kwani alionekana kutojua utaratibu usio rasmi na wa kibabe ambao umekuwa ukitumiwa na makondakta wa magari ya kutoka na kwenda Arusha kuongeza nauli kila ilipofika iliyoitwa jioni.
‘’We umeibiwa pale jijini umepelekwa na wahuni kwenye gari halafu unaniletea u much know hapa’’Aliendelea kujigamba yule kondakta na kuondoka akikusanya nauli kutoka kwa abiria wengine ambao wengi waliokuwa wageni walionekana kushangazwa na utaratibu huo kuna ambao hawakuwa na hela ya ziada waliamua kumbembeleza kondakta kwa kudai kutojua na alipokea pesa zao baada ya kuwakashifu sana kitu ambacho kilinikera lakini sikuwa na cha kuongea kwani bado nilikuwa nikirejewa na taswira na kijana omba omba ambaye bila kujua nilijikuta jina la MTU-JITU likiwa kama jina lake kutokana na kuwa kiumbe aliyetisha sana kwa mwonekano lakini alikwa akiishi miongoni mwa binadamu wengine.
Nilikuwa na uhakika kuwa kulikuwa na jambo kubwa baya lilimpata maishani mwake na hapo nikajikuta kilijiapiza kuwa NITARUDI ARUSHA bila kujua nilikuwa nimetamka maneno hayo kwa sauti iliyowafanya wengi kunigeukia.
‘’Unarudi kwa sababu nimeongeza nauli ama? Na wewe dada nikirudi nikute umeniandalia Buku tatu yangu na jero ya usumbufu’’Aliongea yule kondakta na kuwafanya watu waangue kicheko.
Baadaye yule dada alitoa shilingi elfu tatu na kumkabidhi kondakta huku akitokwa na maneno.
‘’Ikutajirishe na siku uwe na gari yako hiyo mia tano, huo ni utapeli tuu kama wanaodai ombaomba wanaufanya na sipandi gari yenu tena’’Aliongea yule dada kwa hasira na kutoa simu yake akibonyeza namba kadhaa na kupiga.
‘’We ndo hujielewi eti nitajirike niwe na gari yangu halafu hupandi gari yetu tena nishatajirika ndo maana ninamiliki hili gari’’Aliongea akiwafanya abiria kuangua kicheko.
‘’Tajiri anakuwa kondakta? Huna hata haya’’aliongea yule binti akionekana bado kuwa na hasira japokuwa alikuwa akijitahidi kuficha hasira zake lakini zilijidhihirisha kwenye sauti yake , sikupata hata jina lililomfaa yule binti zaidi ya jina SIKUJUA.
Basi baada ya ubishi kati ya Sikujua na yule kondakta ukimya ulichukua nafasi hadi pale mazungumzo ya watu wawili yalipokuja kusikika gari zima na kuvuta wengi waliokuwa wakisikia mazungumzo yao. Alikuwa Mwana USDM akiongea na kijana aliyekuwa jirani yake huku wakisimuliana visa mbali mbali vya omba omba.
Mwana UDSM alisimulia kisa cha yule mama ambaye alikuwa akiomba chuoni UDSM huku akijfanya bubu pale alipokutana naye kwenye chuo kimoja mkoani Iringa na alipomshtua kwa ishara kuwa je , ni yeye wa mlimani alimtuliza kwa kumwekea kidole mdomoni kuwa asizungumze chochote. Alichokifanya ni kuondoka huku akijutia elfu tano zake kadhaa alizowahi kumpa huyo mama aliyeamua kuwaibia wanafunzi mchana kweupe bila kutumia nguvu kubwa.
Yule mwenzake alimsimulia kisa cha mzee mmoja ambaye hana ulemavu wala ugonjwa wowote lakini yupo mjini Moshi na asubuhi huamka na kutembea mwenyewe hadi maeneo ya posta ambapo hukunja mguu wake na kuanza kuomba kana kwamba ni mlemavu na wengi wamegundua na wageni ndio hujikuta wakiingia mkenge kumpa chochote mzee huyo mwenye nguvu ya kufanya shughuli nyingine.
‘’Mie huyo ndiye aliyenifanya niwachukie hao watu maana nilimpa sana pesa kila nilipoenda posta nilipokuja kusimuliwa hilo nilichukia sana na bahati mbaya nilimwona kwa macho yangu akitembea vizuri kabla ya kuangaza huku na huko na kukaa chini kama vile mlemavu wa mguu na mkono mmoja’’Alidakia yule Mwanasiasa ambaye mada ile kama ilimvutia kuliko wote akitetea alichomfanyia yule kijana kule Arusha.
Msomi wa mlimani naye akadakia na kuongeza lake wakati huo akifunua hata shuka alilokuwa amejifunika na yule msichana ambaye alionekana kuzama kwenye kusikiliza muziki uliokuwa ukisikika kwa mbali kutoka kwenye ear phones alizokuwa amevaa.
‘’Mwenyewe kuna omba omba mmoja kule Dar nilishuhudia akiomba hela na baada ya dakika kama kumi nilikutana naye akinywa kiroba. Siku nyingine si akaniomba pesa nikamuuliza nikupe pesa ama nikakununulie kiroba? Mbona alipotea kama upepo hawa wezi sana’’
‘’Wengine huwatumia wazee wao ama watoto wao kuomba omba na hata kujibadika vidonda bandia ili waombe pesa’’Aliongeza mama mwingine aliyekuwa kimya tangu mwanzo wa safari lakini aliamua kutoa la moyoni mwake huku wengi wakionekana kuwalaumu omba omba na kunifanya nijiulize maswali mengi juu ya kundi hilo la watu ambalo si tuu Afrika bali hata kwenye nchi nyingine zilizoendela ambapo visa vya akina Balotelli vilithibitisha uwepo wa omba omba hata kwenye nchi hizo.
Lakini mwisho wa mawazo yangu nilijikuta nikijiuliza , ni kipi kilimpata Yule MTU-JITU wa Arusha? Sikuwa na jibu zaidi ya kuamua kwa mara nyingine tena kuwa NITARUDI ARUSHA safari hii sikutamka kama awali.
Hatimaye tulifika Moshi mjini na hapo nilishuka na haraka haraka nikaelekea kwenye magari yaliyokuwa yakielekea chuo cha maliasili cha MWEKA ambako nilikuwa nikisoma hapo.Baaada ya saa moja ya kubanana kwenye daladala nilifika chuoni na moja kwa moja nilielekea Hosteli ambako nilioga na kulala hadi siku ya pili ambayo ilikuwa ni siku ya jumapili.
Siku hiyo sikuenda kanisani kama ambavyo wenzangu wengi walifanya wakisema uchovu kama sababu ya wao kutoenda kanisani tukiungana na wanachuo wengine ambao jumapili haikuwa siku ya ibada.
Nilikumbuka kuwa nilijipa kazi ya kurudi Arusha, hivyo niliandaa tena kwa safari ya kwenda Arusha bila kumwambia mtu yeyote kwani niliamua kuifanya safari ile kuwa safari ya siri.Sikuwa na sababu nyingi za kuifanya safari ile kuwa siri zaidi ya kutotaka yeyote ajue kilichokuwa kikinirudisha Arusha kwani nilijua wengi wangeniona mtu wa ajabu sana kufuatilia kitu ambacho wangeamini kuwa kilikuwa hakinihusu.
Saa nne na nusu ilinikuta nikiwa kwenye gari la abiria lililokuwa likielekea Arusha huku kichwa changu kikiwa na mawazo mengi sana, nilikaa kimya hadi pale niliposhtushwa na sauti ya kondakta aliyenitania na kufanya watu wacheke na kunigeukie.
‘’Kumbe sikukuelewa ile jana uliposema ungerudi Arusha kumbe ulifurahia huduma zetu?’’ Aliongea kondakta ambaye baada ya kumtazama niligundua kuwa nilikuwa nimepanda tena kwenye gari nililokuwa nimepanda jana yake.
‘’Umeona sasa, wengine waliapa kutopanda gari yetu lakini wewe umeamua kupanda tena , karibu sana leo nakupunguzia mia tano kwenye nauli utatoa elfu mbili tuu’’Aliongea yule kondakta na kuwafanya watu wacheke sana nami nikatabasamu kisha nikainama.
Nilipompa nauli yule kondakta alinirudishia shilingi mia tano huku akinikumbusha kuwa alikuwa amenipunguzia nauli na angenilipia yeye , napo sikusema kitu zaidi ya kutabasamu na kumshukuru.
Nilipofika eneo ambalo nilikuwa nimemwona yule omba omba jana yake niliamua kushuka na kutembea kwa miguu nikiangaza macho huku na huko nikiwa na kibegi changu kidogo mgongoni.
Nilitembea kwa dakika kama kumi na tano hivi bila kumwona MTU –JITU niliyekuwa nimemfuata nikiwa na zawadi zake kadhaa kama vile dawa ya meno, mswaki, nguo mafuta ya kupaka na kiasi kidogo cha fedha nikiwa na matumaini ya kutaka kujua kilichomfanya akawa kwenye hali ya UMTU-JITU.
Baada ya kuzunguka sana nikaamua kujipumzisha kwenye mgahawa mmoja kwani jua lilikuwa likichoma sana siku ile nikishangaa hali ya jiji lile lilivyo kwani jana yake kulionekana na tishio la mvua lakini siku ile palikuwa na jua kali sana.
Nikiwa pale mgahawani ambapo nilikuwa nikinywa maji ya baridi niliyokuwa nimenunua ili kupooza joto la mwili wangu nilikiona kitu ambacho kinipa matumaini na kufanikisha kilichokuwa kimenirudisha Arusha.
Alikuwa mtoto mmoja wa umri wa miaka kati ya tisa na kumi na moja akipita kwenye meza za wateja akiomba chochote.Wengi walionekana kukereka sana na usumbufu aliokuwa akiwaletea kutokana na mwonekano wake ambapo asilimia tisini na sita ya mwili wake ilikuwa imetawaliwa na uchafu na asilimia nne tuu ambayo ni mboni zake na viganya vyake vilionekana vikiwa salama.
Wateja wengi ambao walikuwa wazungu walionekana kukereka sana na kumwita mhudumu ambaye alikuja kumtimua akimwita kwa jina la John .
‘’Kumbe anajulikana?’’Alihoji mteja mwingine wakati huo John alihamia upande mwingine wa mgahawa ule ambao ulikuwa ni wa hadhi ya juu nako alifukuzwa na kuamua kutoka akipita karibu na meza niliyokuwa nimekaa kutoka nje.
Kwa haraka haraka nilimwita mhudumu na kumlipa hela yake kisha nikatoka nje nikiangaza macho huku na huko nikimtafuta John.Niliita jina lake baada ya kumwona amejificha nyuma ya pipa la takataka lililokuwa nyuma ya ule mgahawa , ajabu licha ya kuwa alikuwa jirani yangu hakuitika hadi nilipomsogelea akataka kukimbia kwa haraka nikamdaka mkono.
‘’Naomba niachie sirudii tena kuomba kaka’’ Alijitetea John.
‘’Mie sikupeleki popote nataka nikuulize kitu John nitakupa zawadi’’ Niliongea kwa sauti ya upole.
‘’Nisamehe kaka wala sitorudia’’Alizidi kujitetea yule mtoto akijitahidi kujinasua mikononi mwangu, hapo nikamweka John kwenye kundi la omba omba ambao wameamua kujiingiza huko kutokana na uvivu wa wakubwa wao.
‘’Shika hii, nataka unielekeze sehemu’’ Nilimkabidhi noti ya elfu tano na kumwona John akiniamini na kuwa mpole, lakini licha ya kuwa mpole niliendelea kumshikilia safari hii nilikuwa sijamkamata kwa nguvu sana japokuwa nilikuwa makini sana.
‘’Kuna mtu mmoja hivi anachechemea hivi, halafu anakovu moja mdomoni anafanya,,,,,’’Sikufanikiwa kumalizia maelezo yangu nilijibiwa na yule mtoto.
‘’Nani kaka Japhet? Kama umenipa hela kuniulizia habari zake basi shika tuu hela yako’’ Aliongea yule mtoto akinishikisha ile hela niliyokuwa nimempa na akitaka kujinasua mkononi mwangu.
‘’Kumbe unamfahamu , niambie basi yupo wapi ni ndugu yangu yule nahitaji kumsaidia’’ Niliamua kujieleza.
‘’Ndugu yako, ndo humfahamu hata jina? Mhh sikuamini nenda tuu kaka’’ Aliuliza yule mtoto akitaka kukimbia.
‘’Ni ndugu yangu namfahamu kuwa anaitwa Japhet nilikuwa nakueleezea alivyo ili iwe rahisi wewe kumtambua namhitaji sana ndugu yangu nataka akapate matibabu’’ Niliongea kwa kirefu.
‘’Tunavyojua Japhety hana ndugu hivyo najua wewe ni wale wale siwezi kukutajia alipo’’ Aliendelea yule mtoto huku akihangaika kujinasua lakini nilizidi kumshika mkono wake mwembamba na hata waliokuwa wakipita njia walijua nilikuwa nimemkamata akitaka kuniiba maana nilisikia sauti ya mama mmoja akisema kutokea upande wa pili wa barabara.
‘’Kamezidi wizi hako kapeleke tuu polisi’’ Lakini si hivyo tuu pia niligundua kuwa MTU-JITU au Japhet kama nilivyomfahamu hapo hakuwa na ndugu hivyo na kufanya safari yangu ya kurudi Arusha kuwa na maana ingawa kauli ya kuwa ‘’wale wale’’ na kukataa pesa yangu ingawa alikuwa akiomba pesa mgahawani iliniachia maswali mengi bila majibu juu ya huyo mtu aliyeitwa Japhet.
Kwa mbali niliiona gari niliyokuwa nikiifahamu ikiwa imewasha taa ya kuonesha kuwa ilikuwa ikitaka kuchepuka upande niliokuwa nimesimama na John na nilipoangalia njia ya kwanza kuchepukia upande ule ilikuwa ni pale mgahawani.Nilichokifanya ni kutoa noti mbili za shilingi elfu kumi nikimpa John nikimtaka noti moja aifikishe kwa Japhet.
‘’Nimwambie amempa nani?’’ aliuliza John.
‘’Joseph,’’ nilimwambia na kumwachia wakati huo ile gari iliingia upande wa mgahwani na kuegeshwa na aliyeshuka alikuwa ni mtu niliyemtegemea ingawa nilikuwa nikijifanya kutokuwa na habari na uwepo wa gari ile mahali pale.
‘’Mambo Joseph’’ alinisalimia Alice huku wenzake wakiingia mgahawani walikuwa jumla wanne, nilijifanya kutosikia salamu ile na kama niliisikia basi aliyeitoa lazima ajue kuwa sikujua kama ndiye niliyelengwa na ile salamu.
‘’We Josee unawaza nini ?’’ Aliuliza Alice akinishika begani nami nikajifanya kushtuka.
‘’Ha! Kumbe wewe nilikuwa mbali sana kimawazo’’ Nilimjibu baada ya kumwona Alice, rafiki yangu ambaye jana yake alinifanya niende Arusha.
‘’Mbona upo hapa?’’ Aliuliza.
‘’Tulikuja na mkuu wa chuo akaniacha hapa akiniahidi kunipitia baada ya nusu saa lakini saa la pili hili linaisha hajanipitia , namba yake ya simu sina nimepiga chuoni nimesikia kuwa ameshafika chuoni hapa nashindwa kuelewa kwa nini na hapa nina mia tano tuu mfukoni’’ nilidanganya.
‘’Sa kwa nini hukunipigia?’’ Aliuliza akionekana kukerwa na kitendo cha kutomtaarifu kuwa nilikuwa Arusha na hata baada ya matatizo.
‘’Kwanza nilijua ulikuwa kanisani, halafu mkuu alinitaka kutoendekeza mambo binafsi wakati nimekuja kwa safari ya kiofisi’’ Niliendelea kujitetea.
‘’Kiofisi ndo kuachana kwenye mataa?’’ Aliuliza kwa kejeli lakini akiwa kama mwenye hasira.
‘’Basi tuu kwenye hii nchi watu wa daraja la mwisho tunateseka sana’’niliongea nikionesha unyonge wangu na kumfanya anihurumie , akanitaka niingie mgahawani akanitambulishe kwa rafiki zake nami bila kusita nikaingia ndani akanitambulisha na baada ya dakika kama tano hivi nilipigiwa simu na haraka haraka nikapata akili nikaikata ile simu na kuweka sikioni kisha nikainuka nikiongea.
Niliporejea nilikuja na taarifa ya kuwaaga na kudai kuwa kulikuwa na gari ambalo nilitakiwa nipande ili linifikishe Moshi, licha ya kupingwa sana na Alice baadaye nilikubaliwa kwa shingo upande baada ya madai kuwa ilikuwa ni safari ya kiofisi zaidi hivyo nilitakiwa kufuata maelezo ya wakuu wangu.Nilisindikizwa na Alice hadi nje ya mgahawa ambapo alinikamatisha noti kadhaa ambazo alidai zingenisaidia mbele ya safari.Nilishukuru na kuaga .
Nilienda moja kwa moja hadi upande wa pili wa barabara ambapo nilipotupa jicho langu ng’ambo bado niliona macho ya Alice yakiwa kwangu , nilimpungia mkono kabla ya kupanda pikipiki iliyokuwa jirani yangu na kutoa maelezo ya kupelekwa kituo kikuu cha magari.
Njiani nilimuuliza yule mwendesha pikipiki kuhusu mtu aliyekuwa na wasifu wa Japhet bila kutaja jina lake naye bila kusita alinijuza kuwa alikuwa ameshawahi kumwona yule mtu lakini hakujua chochote kumuhusu kwani hakuwa mwenyeji sana na lile jiji.
Nilipofika kituo kikuu cha mabasi nilimlipa yule jamaa wa pikipiki kisha nikaanza kuzunguka zunguka nikimtafuta Japhet ambaye ndiye aliyenirudisha Arusha.Nilitumia zaidi ya nusu saa bila mafanikio yoyote hadi nikaanza kukata tama.Nikaona nitumie tena njia ya kuwauliza omba omba waliokuwa maeneo yale ajabu kila niliyekuwa nikimuulizia kuhusu Japhet alionekana kumfahamu lakini akikataa kuongeza chochote kumhusu jambo ambalo lilinifanya nihisi kuwa kulikuwa na kitu kilichokuwa kimejificha kwenye maisha yake.
‘’Kiukweli ninavyomfahamu huyo mtu ni hivyo nilivyokueleza, hakuna kingine ninachokifahamu hata ukanipa mamilioni ili niachane na huku kuomba siwezi kukuambia kingine maana sijui’’Aliongea mzee mmoja omba omba akitetemeka na kunifanya nianze kupata uoga kufuatilia maisha ya Japhet ambaye baadaye nilikuja kugundua kuwa halikuwa jina lake halisi kwani katika watu kumi niliowauliza walinitajia majina mengine matano tofauti.
Nilichoka. Lakini kitu cha ajabu ni kuwa kadri ugumu wa lile jambo lililokuwa limenirudisha Arusha ulivyoongezeka ndivyo hamu ya kutaka kujua zaidi juu ya Japhet ilivyoongezeka mara dufu.Niakaamua kupita kwenye kituo cha magari madogo ya usafiri maarufu kama vifodi ili kuendeleza utafiti wangu usio rasmi.
Wakati naelekea huko nikikaribia kufikia barabara ingiayo kwenye kituo cha Vifodi nilimwona John na Japhet wakitokea nilikokuwa nikielekea na kwa maana hiyo tungekutana baada ya mimi kuvuka barabara iliyokuwa ikielekea mjini.Waliponiona walionekana kuelekezana kitu na hapo nilimwona Japhet akiniangalia sana kana kwamba aliwahi kuniona sehemu.
Kwa haraka bila umakini nikaingia barabarani nikikimbia kuelekea ng’ambo ya barabara kuwafuata akina Japhet, nilikuja kushtuka nikiwa nimebakiza hatua mbili ili niwe ng’ambo ya barabara baada ya kusikia kelele za watu na matairi ya gari yakilalamika.Nilipoinua uso wangu kuangalia kushoto kwangu nilikutana na macho makali ya mtu akiwa garini akiwa haamini kama alikuwa amenikosa kunikanyaga na gari yake.
‘’We Joseph utanipa kesi bure’’ Aliongea Alice ambaye nilikuwa nimeachana naye mgahawani, kwa kuwa akili yangu ilikuwa ni kuonana na Japhet nilijikuta nikigeuzia uso wangu pale nilipokuwa nimewaona Japhet na John lakini sikuwaona zaidi nilikutana na kundi kubwa la watu wakishangaa ile ajari ambayo ilitaka kutokea lakini ilisababaisha msongamano mwingine.
Nilirudisha uso wangu kwa Alice wakati huo nikiwa pale pale barabarani nikiwa nimepiga magoti mikono nikiwa nimeishikilia ardhi kana kwamba nilikuwa nikiizuia kupanda juu zaidi.
Nikajikuta nikipata cha kutamka.
‘’Nimechelewa gari tena’’
‘’Nitakupigia’’Alinijibu na kuondoa gari yake kuzuia kutokea kwa msongamano zaidi wa magari.
Niliinuka na kujichanganya kwenye kundi la watu kwani askari wa usalama wa barabarani walikuwa wakiwasili eneo lile hivyo niliona hatari ya kujiingiza kwenye matatizo mengine.
Nilipita kwenye njia kadhaa na kujikuta nipo kituo kikuuu cha magari ambapo nilidandia gari moja iliyokuwa ikitoka kituoni kuelekea Moshi mjini hakukuwa na siti iliyokuwa wazi hivyo nilisimama nikisubiri kupata siti baada ya abiria wengine kushuka.
Simu yangu iliita na mpigaji alikuwa Alice , nilipokea na kumweleza kuwa nilikuwa garini kuelekea Moshi na aliponitaka nimweleze kilichotokea hadi nikachelewa gari nika mjibu kwa kifupi, ‘’Usijali Nitarudi Arusha ‘’ nikakakata simu na kuiweka mfukoni.
Njiani nilipata mawazo mengi juu ya maisha Japhet ambaye awali nilimwona kama MTU-JITU kutokana na mwonekano wake, nilihisi kuna kitu kilichomfanya akawa MTU-JITU na kitu hicho si kidogo kutokana na hofu waliyokuwa nayo niliokuwa nimewauliza juu yake hapo nikajikuta nikijiapiza akilini kuwa NITARUDI ARUSHA.

Tagged as: ,
Unknown About Unknown

“You have no idea how much the last few days have meant to me," I began. "Meeting you has been the best thing that's ever happened to me.” Get the latest entertainment updates from Best Hope Media or call +255 655 987 588

Get Updates

Subscribe to our e-mail newsletter to receive updates.

Share This Post

Related posts

0 comments:

Like, share and send to friends