UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU
UTANGULIZI
Wizara imekusanya maoni ya Wadau wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.
Muundo wa Kwanza ni upangaji wa viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade Ranges) zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.
Muundo wa Pili ni wa viwango vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini kuanzia mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando (Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama mgando ambapo: A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa upande wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu ya malalamiko katika sekta ya elimu na mafunzo.
Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho utachangia asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa kujitegemea (private candidates). Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.
Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria kufanya harmonization ya masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi katika ngazi mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika ngazi mbalimbali.
VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA MWAKA
2014 KIDATO CHA SITA
2014 KIDATO CHA SITA
Baada ya kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu makundi ya alama na muachano wake:
a) Alama zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana, isipokuwa tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.
b) Makundi ya alama hayatakuwa na clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija katika kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii
(i) makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters mbili. Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka 59 na litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50 hadi 59 na kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).
(ii) Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna haja ya kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika kundi hili.
(iii) Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama 20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa chini kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha. Alama F ilikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia alama 20 hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu ni kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.
c) Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0 hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo zitakatumika
(i) Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance),
(ii) Alama B+ itakuwa na maana ya ufaulu bora sana (excellent performance),
(iii) Alama B itakuwa na maana ya ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),
(iv) Alama C itakuwa na maana ya ufaulu mzuri (good performance);
(v) Alama D itakuwa na maana ya ufaulu wa wastani (low performance),
(vi) Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii) Alama F itakuwa na maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).
Wataalamu katika maeneo mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na Wizara, watatoa maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji yao.
d) Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alamaD na E ni alama za ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya eneo husika (targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.
e) Makundi ya alama yatajumuisha CA kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.
f) CA kwa upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya Kidato cha Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama 10) na kazi mradi au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.
g) CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegmea ambao wanarudia Mitihani, CA zao zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya awali. Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya QT yatumike kama CA na mtihani wa mwisho uchangie alama 60.
h) Kwa vile alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013.
i) Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) utaandaliwa na kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa kuhusu muundo huo ili wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya sekondari.
j) Muundo huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.
Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:
Jedwali Na 1
MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU
ALAMA | UWIGO WA ALAMA | IDADI YA ALAMA | TAFSIRI |
A | 75 - 100 | 26 | Ufauli Uliojipambanua |
B+ | 60 - 74 | 15 | Ufaulu bora sana |
B | 50- 59 | 10 | Ufaulu mzuri sana |
C | 40 - 49 | 10 | Ufaulu mzuri |
D | 30 - 39 | 10 | Ufaulu Hafifu |
E | 20 - 29 | 10 | Ufaulu hafifu sana |
F | 0 - 19 | 20 | Ufaulu usioridhisha |
Kwa aina hii ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika kipindi hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja utakuwa kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 2 hapa chini.
Jedwali Na 2
MUUNDO WA MADARAJA
MUUNDO WA ZAMANI | MUUNDO MPYA | MAELEZO | ||
POINTI | DARAJA | POINTI | DARAJA | |
7-17 | 1 | 7-17 | I | Kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana |
18-21 | II | 18-24 | II | Kundi la ufaulu mzuri sana |
22-25 | III | 25-31 | III | Kundi la ufaulu mzuri na wa wastani |
26-33 | IV | 32-47 | IV | Kundi ufaulu hafifu |
34-35 | 0 | 48-49 | V | Kundi la ufaulu usioridhisha |
Wataalamu wa mifumo ya mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili liweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika ufaulu.
HITIMISHO
Mabadiliko haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu. Masuala haya yanaendelea kuangaliwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN). Ushirikiano wa wadau wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara itaendelea kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia wanaombwa wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo lolote ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata mafanikio katika sekta ya elimu.
Imetolewa,
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
0 comments: