Mambo muhimu ya kuyafahamu katika siku ya wapendanao

on Saturday, February 13, 2016 - No comments:

Siku ya Wapendanao siyo kwa ajili ya kufanya ngono au uzinzi.Hii ni siku inayolenga kuimarisha upendo kati yako na mtu mwingine yeyote. Picha na Maktaba


Kwa ufupi

Siku ya wapendanao ni sikukuu ambayo huadhimishwa ifikapo Februari 14 kila mwaka. Historia yake imeanzia karne ya tatu nchini Italia.

Kuna wanaume na wanawake, leo ni sherehe yao ya kufanya ngono/uzinzi, wakifikiri kwamba ndiyo maana ya siku hii ya Valentine Day, kitu ambacho si kweli.Usahihi ni kwamba siku hii imelenga kuhamasisha watu kupendana, ndiyo kusema kwamba unaweza kuonyesha upendo kwa mtu yeyote, si lazima awe mwenza wako.

Nchini Italia wakati huo kulikuwa na kiongozi aliyeitwa Mfalme Claudius II; aliamini kuwa askari anapooa hawi mkakamavu na pia muda mwingi anawaza kuhusu familia yake zaidi ya kitu kingine chochote. Hivyo alipiga marufuku ndoa kwa askari.

Kitendo hicho hakikuwafurahisha watu wengi, akiwamo Padri Valentino. Kiongozi huyu wa kidini aliendelea kufungisha ndoa kwa siri. Mfalme Claudius alipopata habari hizi aliamuru Valentino akamatwe na kuuawa. Mtakatifu Valentino aliuawa siku na tarehe kama ya leo, ndiyo maana ikatangazwa rasmi kuadhimishwa kwa ajili ya kumkumbuka kama Baba wa Upendo na mtetezi wa wanandoa. Historia zinaonyesha kuwa aliyetangaza rasmi kuadhimisha siku hiyo ni Papa Gelasius.
Aidha, iko simulizi nyingine inayosema kuwa akiwa gerezani Valentino aliandika barua ambayo ilikuwa na salamu za Valentino kwa binti aliyekuja kumsalimia gerezani; mwisho wa barua alihitimisha kwa kusema ‘Kutoka kwa Valentino wako’.
Tangu hapo Valentino anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake kuadhimishwa ulimwenguni kote.


ZAIDI KUHUSU SIKU HII

Siku hii inaonekana ni maalumu kwa ajili ya kuonyeshana upendo wa dhati kwa mtu yeyote. Ni siku muhimu na yenye maana kubwa kwa kila mtu, maana upendo hauchagui.

Ingawa wengine wanaweza kuitumia au kuichukulia kwa kadri wanavyotaka, msingi wa siku hii hasa ni kuonyesha upendo kwa watu, si lazima awe mke au mumeo ama mchumba.

Maana na ukweli wa uwepo wa siku hii inayoitwa Valentine’s Day inaharibiwa na baadhi ya watu kwa kuiona kama ni siku ya kufanya ngono/uzinzi. Ukitaka kuthibitisha hili, siyo lazima uende chuo kikuu ili kupata ujuzi wa kujua ukweli, bali tembelea nyumba za wageni zilizo karibu, nyingi utakutana na bango ‘vyumba vimejaa!’

NAMNA INAVYOPASWA

Msingi hasa wa siku hii ni kuonyesha upendo, hii ina maana kuwa unaweza kuonyesha upendo kwa yeyote iwe ni jirani, mzazi au yeyote unayempenda, siyo lazima mpenzi kama ambavyo baadhi ya watu wanafanya.

Waweza kumtumia ujumbe mzuri mtu yeyote unayempenda au hata zawadi, waweza kutembelea yatima, wagonjwa na hata watu wengine wowote; kubwa hasa kwa siku hii ni kuonyesha upendo.

Hata hivyo, kwa sababu ya ukweli kwamba wengi wanaiona kama ni siku ya ngono, ni suala la msingi sana unapotoa zawadi kwa mtu wa jinsi tofauti kuwa makini; angalia zawadi unayoitoa isije ikaharibu siku yako na maisha yako kwa jumla badala ya kukupa furaha, kwa sababu baadhi ya wenza wa wale ambao unaweza kuwapa zawadi wanaweza kutafsiri kama wewe una uhusiano wa kimapenzi na mtu huyo.

Wataalamu mbalimbali wa masuala ya uhusiano, wanasema katika siku kama hii ya leo, ni vizuri walio kwenye uhusiano mbaya kujifunza namna ya kuwa na uhusiano mzuri, kwani ubaya hauna maana katika maisha.

“Hii ni siku muhimu kwa kila mtu kuangalia uhusiano wake na watu wanaomzunguka,” anasema Hi Song, ambaye ni Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano nchini Marekani kutoka Kituo cha Ushauri cha Marriage Life. Anasema kuna ambao huanzisha uhusiano siku hiyo kwa lengo la kupata mtu wa kustarehe naye, hili ni kosa. Kama mtazamo wako ni kutafuta mpenzi mpya na kwenda kustarehe naye utakuwa unakosea sana. Haina maana ya ngono wala anasa na kuharibu fedha kwenye ulevi. Yapo mengi ambayo unaweza kuyafanya kwa lengo la kuifanya siku yako kuwa nzuri.

ONDOA MAWAZO MABAYA

Ondoa fikra mbaya kichwani mwako. Waza kuhusu mema na kupendana kwa dhati, hapo utakuwa umekwenda sawa na maana ya siku hii. Kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wazee na wahitaji wengine. Tumia ulichojaliwa kushiriki nao katika siku hii ya leo, badala ya kuwaza ngono au uzinzi.

Siyo lazima iwe fedha, hata chakula na mavazi. Inawezekana una nguo unazodhani hazifai, wape wenzako ambao wanahitaji hapo utakuwa umeonyesha namna unavyotambua na kuiadhimisha kwa usahihi.

By Dismas Lyassa, Mwananchi

Tagged as:
Unknown About Unknown

“You have no idea how much the last few days have meant to me," I began. "Meeting you has been the best thing that's ever happened to me.” Get the latest entertainment updates from Best Hope Media or call +255 655 987 588

Get Updates

Subscribe to our e-mail newsletter to receive updates.

Share This Post

Related posts

0 comments:

Like, share and send to friends