Siku ya kimataifa ya vijana: nini mchango wavijana katika ujenzi wa taifa?

on Friday, August 12, 2016 - No comments:


Na: William Haule Tematema,
Mwenyekiti, 
Jukwaa la Mijadala, Tafiti na Ushauri.

Mnamo tarehe 17/12/1996, Umoja wa Mataifa ulipitisha na kuitangaza tarehe 12 ya mwezi wa 8 kila mwaka kuwa ni siku ya kimataifa ya vijana. Hivyo tarehe 12/08/2016 , vijana wa Tanzania wanaungana na vijana wenzao wa ulimwenguni kote kusheherekea siku hii. Kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya siku hii ya vijana inasema 'Kuelekea 2030: Tutokomeze umasikini ili tufikie malengo ya uzalishaji na matumizi endelevu'.

Uzalishaji endelevu ni uzalishaji wa huduma au bidhaa kwa kutumia michakato (processes) na mifumo (systems) ambayo haiharibu mazingira, inatumia nishati na maliasili kwa kiasi kidogo, inaleta faida kubwa ya kiuchumi, ni salama kwa wafanyakazi, watumiaji na jamii kwa ujumla.

Matumizi endelevu maana yake ni kitendo cha kutumia rasilimali au huduma zilizozalishwa kiasi cha kutosheleza kizazi cha sasa na kuacha akiba ya rasilimali au huduma hizo kwa kizazi kijacho. Kwa lugha nyingine ni kuwa, maendeleo ya kesho yanapaswa kuandaliwa leo, na maendeleo ya keshokutwa yanapaswa kuandaliwa leo na kesho. Maendeleo endelevu ni zao la fikra endelevu, uzalishaji endelevu na matumizi yenye mipaka.

Kwa mujibu wa sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 1996 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2007, kijana ni mtu mwenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya Tanzania ya mwaka 2012, vijana ni zaidi ya asilimia 35 ya watanzania wote.
Katika taifa lolote lile, vijana ni nguzo muhimu katika shughuli na masuala mbalimbali, iwe ni shughuli za ujenzi, vita, siasa, n.k. Vijana wana hamu, shauku, ndoto na matumaini makubwa ya maendeleo, huku wakiwa na nguvu nyingi na akili zao zikiwa zinachemka.

Lengo kuu la kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya vijana ni kuhimiza vijana kuwa mstari wa mbele katika kufikia malengo ya Ajenda ya 2030 ya Maendeleo endelevu. Hivyo, kaulimbiu hii inawakumbusha vijana wa kitanzania kuwa, wana nafasi kubwa ya kuchangia au kulisaidia taifa lao kuyafikia maendeleo endelevu, kwa njia mbalimbali. Je ni mambo gani vijana wanapaswa kufanya ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu?

Kwanza, vijana wa kitanzania wanapaswa kuwa na fikra yakinifu. Ufikiri yakinifu ni suala muhimu sana kwa vijana. Ufikiri yakinifu ndio hupelekea uvumbuzi na ubunifu wa vitu na mambo mbalimbali. Kama ambavyo John F. Kennedy, Rais wa Marekani miaka ya 1961 - 1963, aliposema "usifikirie kuwa nchi yako itakufanyia nini, ila fikiria utaifanyia nini nchi yako".Hii inamaanisha kuwa vijana wanatakiwa kuja na mawazo mapya yenye maendeleo chanya kwa taifa. Lakini pia vijana ni lazima wajue umuhimu wa kusoma, kwa kuwa kusoma au kujisomea ndio hupelekea kuwa na fikra yakinifu na upeo mpana. Kuna usemi wa lugha ya kingereza unaosema "the reading nation, is the leading nation". Kwa tafsiri isiyo sahihi ya usemi huu ni kwamba, 'taifa linaloongoza, ni taifa lenye watu wanaosoma'. Ukweli katika hili ni kwamba, vijana wa kitanzania ni wavivu wa kusoma, na hata wale wachache wanaosoma, husoma kwa kujifurahisha. Kupitia kusoma, ndipo unaweza kupata mawazo mapya ya maendeleo yatakayobadili taifa letu. Vijana watakuwa wadau wazuri na viongozi bora wa taifa, endapo watakuwa wanajua mambo mengi hususani yanayohusiana na maendeleo, jambo ambalo linahitaji kujifunza kupitia kujisomea kwa kila siku.

Pili, vijana wanapaswa kuwa wabunifu. Gurudumu la maendeleo la taifa lolote, hutegemea sana ubunifu na uzalishaji wa vijana wa taifa hilo. Hii inamaanisha kwamba, taifa ambalo vijana wake hawafikiri, si wabunifu na ni wavivu katika uzalishaji mali, taifa hilo kamwe haliwezi kuendelea. Kila kona ya nchi kwa sasa, vijana wengi wanalia na tatizo la ajira, jambo ambalo nakubaliana nalo kwa asilimia mia moja. Lakini kwa upande mwingine vijana wanapaswa wakumbuke kanuni ya kwanza ya mwendokasi ya Isaack Newton inasema, "hakuna kitu kinachoweza kujongea kutoka sehemu moja kwenda nyingine, pasipo kutumika nguvu". Tafsiri ya kanuni hii, inaweza kuwa inakatisha tamaa hasa kwa wale wanasubiri kuajiriwa. Lakini huo ndio ukweli. Huu ni muda wa vitendo. Ni muda muafaka wa vijana kupanua wigo wa kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa taifa, kwa kufanya ujasiriamali, kilimo, au ufudi stadi. Vijana hawapaswi kusubiri hadi wawe na mtaji mkubwa ili kuanzisha biashara. Wanaweza kuanza biashara kwa mtaji mdogo wa fedha, ambapo kutokea hapo wanaweza kukuza mitaji yao na hatimaye kuzifikia ndoto zao. Kuwekeza na kufanya biashara katika sekta zinazoajiri na kuleta faida kubwa kama sekta za kilimo, viwanda, usafirishaji, mawasiliano, n.k.

Tatu, vijana wanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko. Vijana ni lazima wawe chachu ya mabadiliko. Na mabadiliko hayo hayana budi kuanzia kwao. Ni lazima watumie uwezo wao kuisaidia serikali katika kutekeleza sera zake, lakini pia lazima wapinge kwa nguvu zote aina zote za unyonyaji unaofanywa na mtu au kundi la watu dhidi ya umma, na pia hata unyonyaji unaofanywa na kundi kubwa dhidi ya kundi dogo au mtu mmoja.

Nne, Vijana wanapaswa kuonyesha mfano mzuri wa aina ya uongozi yenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho. Vijana ni lazima washiriki katika kufanya maamuzi kwa kujiunga na kushiriki katika siasa. Kada ya uongozi ilikuwa imetawaliwa kwa kiasi kikubwa na wazee ambao walidhani kuwa suala la kujenga na kulitumikia taifa, ni jukumu lao na si la vijana, kwa madai kuwa vijana ni taifa la kesho. Lakini hiyo kesho mara nyingi ilikuwa haifiki. Kauli na misemo kama hii imewafanya vijana wakae pembeni na kuacha kushiriki pamoja na kutimiza majukumu yao wakidhani kuwa muda wao wa kutimiza majukumu kwa taifa bado. Taifa lenye vijana wanaojitambua, ni taifa litakaloendelea, na taifa lenye vijana wasiojitambua ni taifa lenye safari ndefu ya maendeleo. Vijana wengi wamedhihirisha kuwa wanaweza kuwa viongozi wazuri au kuwa na mchango mkubwa katika taifa, ili hali wana umri mdogo. Mfano Mwl. Nyerere, alianza kuongoza harakati za kudai Uhuru akiwa na miaka 30, na akaanza kuhudumu nafasi ya Urais wananchi akiwa na miaka 39. Salim Ahmed Salim alihudumu kama balozi wa Tanzznia nchini Misri akiwa na miaka 22. John Samuel Malechela alihudumu kama balozi wa Tanzania kuwakilisha Umoja wa Mataifa akiwa na miaka 28, huku Jenerali Mrisho Sarakikya alikuwa Mkuu wa Majeshi akiwa na miaka 30. Bila kumsahau Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa vipindi viwili tofauti. Vijana hawa wote walihudumu nafasi zao kwa weledi na uwezo mkubwa.

Tano, vijana wanapaswa kuwa na uzalendo kwa taifa lao. Kwa sasa, uzalendo ambayo ni tunu muhimu sana, imepotea miongoni mwa vijana wengi. Ili taifa liweze kustawi, ni lazima watu wake wakiwemo vijana, wawe na mapenzi ya dhati na yasiyo na mipaka kwa taifa lao. Maovu yote yanayofanyika katika taifa hili, kama vile rushwa ufisadi, ukwepaji kodi, utakatishaji fedha, na mengine mengi, ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo. Kama vijana wa kitanzania, uzalendo ni lazima uonekane katika maisha yao ya kila siku. Uzalendo unapojengeka ndani ya mioyo na akili za vijana wa kitanzania, itawafanya vijana hao waone kuwa Tanzania ni mali yao, na hivyo ni jukumu lao kuilinda. Watatumia nguvu zao, akili zao na ujuzi wao kulijenga taifa lao kwa maslahi ya kizazi chaleo na kesho. Kama vijana watakuwa wazalendo, wataweza kupinga rushwa na aina zote za uhujumu uchumi, na hata siku wakipewa dhamana katika ofisi za serikali au taasisi binafsi, wat aendelea kuyapinga maovu.

Sita, Vijana wanapaswa kufanya kazi kwa bidii. Vijana ni kama injini ya gari. Bila injini, gari haliwezi kutembea. Vivyo hivyo, taifa bila vijana, haliwezi kuendelea. Kundi la vijana ni uti wa mgongo wa taifa. Vijana ni injini ya uzalishaji na maendeleo, kwa kuwa ndiyo nguvukazi katika uzalishaji wa mazao, bidhaa au huduma. ⁠⁠ Hivyo wanapaswa kuwa wepesi wa kujifunza, kufanya kazi katika mazingira magumu na yenye presha, na kuleta mafanikio makubwa katika taasisi au taifa.

Saba, vijana wanapaswa kuwa mabalozi wa kusambaza kabari mbalimbali zinazohusu maendeleo. Ni lazima kuwe na taasisi za vijana ambazo ni kubwa na zenye nguvu, ambazo zitakuwa ni majukwaa ya vijana kujihusisha na shughuli za ujenzi wa Taifa ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kuhusu maendeleo ya taifa lao na Tanzania ya lwo na kesho. Mfano, kwa sasa tunazungumzia utekelezaji wa maendeleo endelevu, lakini katika uhalisia zaidi ya nusu ya watanzania hawajui kama kuna kitu kinaitwa Ajenda ya Maendeleo Endelevu. Hivyo katika mazingira haya, nchi haiwezi kufikia malengo hayo ya maendeleo endelevu.

Lakini kwa upande mwingine pia, serikali na jamii kwa ujumla pia haipaswi kukaa nyuma katika kuwajengea vijana katika kuchangia kuleta maendeleo maendelevu. Vijana wanatakiwa kufundishwa maarifa na ujuzi unaoakisi maendeleo ya taifa husika. Pia vijana wanapaswa kujua kusoma, kuandika, kufikiri, kuchambua na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu taifa hilo. Baba wa taifa la Afrika Kusini, Hayati Nelson Rolihlahla Mandela (Madiba), alipata kusema kuwa "hakuna taifa linaloweza kuendelea, pasipo na kuelimika kwa watu wake".

Nguvu na upeo wa akili za vijana, ni kama tochi inayomulika maendeleo ya Taifa. Katika dunia ya leo, maarifa na ujuzi ndio vimekuwa sarafu (fedha) ya dunia nzima. Lakini hakuna benki kuu ya sarafu hii, bali ni viongozi na jamii ndio hupanga jinsi ya kuzalisha sarafu hii, na jinsi ya kuitumia. Taifa linaweza kuwa na utajiri wa rasilimali kama gesi asili, madini au mafuta, lakini rasilimali hizi zinaweza kuwa hazina maana endapo faida inayotokana na rasilimali hizo, hazitawekezwa katika sekta muhimu kama elimu ambayo ndio shamba la fikra mpya.

Pia ni lazima taasisi zetu za elimu, hususani vyuo vya ufundi, vyuo vya kati na vyuo vikuu, viwaandae wahitimu wao kuwa watengeneza ajira na siyo kuwa wanasubiri kuajiriwa. Kijana anapoanza masomo ya chuo, anapaswa kujua kuwa atakapohitimu hapaswi kufikiria kuajiriwa au kurudi nyumbani na kuwategemea wazazi.

Nchi yetu kwa sasa imeathiriwa sana na siasa, hususani zisizo na tija. Wito wangu kwa wanasiasa wote ni kuwa, wanapaswa watambue kuwa wana jukumu la kuwajenga vijana, na siyo kuwatumia kwa maslahi yao binafsi kama vile kuwashawishi kufanya vurugu, maandamano yaliyo kinyume na sheria, n.k.
Mwisho, Kuna misemo inayosema kuwa "ukishindwa kupanga, unapanga kushindwa" na mwingine ukisema "vijana ni taifa la leo na kesho". Kama kweli vijana ni taifa la leo na kesho, basi leo ndio muda muafaka wa kuliandaa hilo taifa. Na kama tutashindwa kupanga kuliandaa leo taifa la kesho, basi tutapanga kushindwa katika taifa la kesho.

⁠Wako comrade,
William Haule Tematema,
Mwenyekiti, 
Jukwaa la Mijadala, Tafiti na Ushauri. 
0657878416
williamhaule99@yahoo.com

Unknown About Unknown

“You have no idea how much the last few days have meant to me," I began. "Meeting you has been the best thing that's ever happened to me.” Get the latest entertainment updates from Best Hope Media or call +255 655 987 588

Get Updates

Subscribe to our e-mail newsletter to receive updates.

Share This Post

Related posts

0 comments:

Like, share and send to friends